Shirikisho la Ngumi za kulipwa la Afrika
(IBF Africa) kwa kushirikiana na Taasisi ya Miss Tanzania 2012,
Brigitte Alfred Foundation (BAF) wameandaa mapambano ya ngumi ya
kimataifa kwa kushirikisha mabondia nyota duniani.
Mapambano hayo yamepangwa kufanyika
Novemba 28 kwenye ukumbi wa Mlimani City na lengo lake kubwa ni kutafuta
fedha za kusaidia watu wenye ulemavu wa ngozi (albino).
Akiongea na millardayo.com Miss Tanzania
2012 Brigitte alisema….“Tumeandaa mbio za Marathon mkoani Kilimanjaro
wiki moja baada ya ngumi, mbio hizo, pia kutakuwa na zoezi la kupanda
mlima Kilimanjaro, lengo ni kutafuta fedha za kuwasaidia albino na vile
vile kutangaza utalii wetu, naomba makampuni yajitokeze,” -Brigitte.
Rais wa IBF Africa, Onesmo Ngowi alisema
kuwa siku hiyo imepewa jina la “knock out albinos killers” (piga wanaua
albino) ambapo bondia kutoka Denmark, Lolenga Mock atapigana na bondia
nyota wa Zambia, Chioctha Chimwemwe katika pambano la uzito wa super
middle la IBF continental Africa super.
Pambano hilo limepangwa kuwa la raundi
12 na litafuatiwa na pambano lingine la kulipiza kisasi kati ya bondia
kutoka Afrika Kusini, Phillip Ndou atakayepambana na Mtanzania, Ramadhan
Shauri kuwania ubingwa wa IBF-Continental Africa welterweight ambalo
pia litakuwa la raundi 12.
Bondia nyota wa Tanzania, Cosmas Cheka
naye atapanda ulingoni kupambana na Gottlieb Ndokosho wa Namibia kuwania
ubingwa wa IBF continental Africa super-feather.
Waandaji wa tamasha hilo wameamua
kushirikiana na Brigitte kutokana na kutambua juhudi zake za kutetea
albino baada ya kuwajengea bweni eneo la Buhangija, Shinyanga na taasisi
yake kwa kushirikiana na Junior Achievements (JA) wanatoa elimu ya
ujasiriamali kwa jamii hiyo.
“Brigitte akiwa mwenye mashindano ya
urembo ya dunia, 2012, aliweka rekodi ya kushika nafasi ya tatu katika
mashindano ya ‘urembo wenye malengo maalum” au Beauty with purpose”,
alipeleka kazi yake ya ujenzi wa bweni la albino mkoani shinyanga,
imetupa faraja sana na kuamua kumuunga mkono katika vita hiyo,”- Onesmo
Ngowi