KAMPUNI
I-View Studios ya mjini Dar es Salaam imeshinda mchakato wa kurekodi video mpya
ya msanii Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’ ambayo usaili wake utafanyika
Jumamosi kwenye ukumbi wa Nyumbani Lounge, Dar es Salaam.
Akizungumza
mjini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Kampuni ya One Touch Solutions, Petter
Mwendapole alisema I-View imepata nafasi hiyo kutokana na kiwango kikubwa cha
video kadhaa ilizofanya lakini pia vifaa ilivyo navyo na uwezo wa wafanyakazi
wake.
“Siku
zote kila mtu anaangalia kitu kizuri, Diamond ametaka kufanya mapinduzi katika
tasnia ya muziki, lakini kufanya mapinduzi kunahusisha vitu vingi, tungo zake
yeye kama msanii, studio anayorekodia watu watakaoshiriki kwenye video yake
kampuni itakayorekodi video pia, lakini mwisho wa siku I-View chini ya Raqey
Mohamed ndio imeshinda nafasi hiyo.
“Raqey
anafahamika kwa kazi zake pamoja na kurekodi matangazo mbalimbali ya
Televisheni, picha mnato lakini pia video za wasanii Taznim ya Kwasakwasa,
Utanikumbuka ya Suma Lee ni baadhi ya kazi ambazo zinaonyesha uwezo alionao
lakini pia Diamond na timu yake tumeweza kuona vifaa vipya na vya kisasa
ambavyo Raqey anavyo kwa sasa na hakuna kwa Afrika Mashariki na Kati,” alisema.
Kwa
upande wake Raqey ambaye ni Mkurugenzi wa I-View alisema anahitaji kuifanya kazi
hiyo kuwa tofauti ili kusukuma mbele sekta ya mawasiliano na muziki kwa ujumla.
“Sisi
kama I-View tunafurahi kufanya kazi na Diamond, ni msanii mzuri na mkubwa
ambaye kazi zake zinaonekana, hatutamuangusha na mashabiki na wasanii wengine
wasubirie kazi itakapotoka,” alisema.
I-View
pia watashiriki katika mchakato wa kupata watu watakaonekana kwenye video hiyo
ambayo ni kwa mara ya kwanza nchini kutafanywa usaili wa washiriki. Usaili huo
utafanyika Jumamosi katika ukumbi wa Nyumbani Lounge ambao unamilikiwa na
mwanamuziki Lady Jaydee. Majina ya majaji wataochuja yatanatarajiwa kutangazwa
leo.