Simba SC
KATIKA kujiandaa na mechi ya Ngao ya Jamii, mabingwa wa Tanzania Bara,
Simba SC, Jumamosi watacheza mechi ya kujipima nguvu na Mathare United
ya Kenya kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha.
Habari za ndani kutoka Simba, ambazo zimepatikana, zimesema kwamba
tayari makubaliano yamefikiwa na timu timu hiyo ya Daraja la Kwanza
Kenya, ambayo ilimuibua kisoka mshambuliaji wa AJ Auxerre ya Ufaransa,
Dennis Oliech.
Simba itamenyana na Azam katika mechi ya Ngao ya Jamii ya kuashiria
kufunguliwa kwa pazia la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Septemba 8,
mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Habari za ndani kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), zimesema
kwamba, kuchelewa kwa mechi hiyo ambako kumeenda sambamba na kuchelewa
kuanza kwa ligi hiyo, kumetokana na kuchelewa kufikiwa mwafaka mapema wa
mkataba mpya wa udhamini wa Ligi Kuu.
Mkataba wa awali wa Vodacom na TFF unafikia tamati mwishoni mwa mwezi
huu na kusainiwa mkataba mwingine, baada ya majadiliano yanayoendelea.
Lakini kwa kuwa Mkutano Mkuu wa TFF uliopita uliridhia kuanzia msimu
ujao Ligi Kuu iendeshwe na kampuni itakayoundwa na klabu za Ligi Kuu
mjadala kuhusu udhamini mpya wa ligi umekuwa mrefu kutokana na kuhusisha
pande tatu, klabu, wadhamini na shirikisho.
Lakini sasa, kwa vyovyote, hata maridhiano ya mkataba mpya wa udhamini
na Vodacom yachelewe tena, mechi hiyo itachezwa Septemba 8, ikiwa ni
wiki moja kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu.
Kihistoria hiyo itakuwa mechi ya tano ya Ngao ya Jamii kuchezwa nchini
na ya pili kuishirikisha timu nje ya wapinzani wa jadi wa soka ya
Tanzania, Simba na Yanga.
Mtibwa ilicheza na Yanga mwaka 2009, baada ya Simba kugoma na ikashinda
mabao 2-1 na kutwaa Ngao, wakati kabla ya hapo, mwaka 2001, Ligi Kuu ya
Tanzania ikiwa bado inadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL),
kupitia bia ya Safari Lager, ilichezwa mechi ya kwanza ya Ngao
kihistoria.
Katika mechi hiyo, Yanga ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Simba na mwaka
juzi Yanga iliifunga tena Simba kwa penali 3-1 kufuatia sare ya 0-0 na
mwaka jana, Simba ilitwaa Ngao ya kwanza katika historia yake, kwa
kuifunga Yanga mabao 2-0.